Makamu wa Askofu asisitiza Katiba bora
MAKAMU wa Askofu Jimbo
la Mashariki Kaskazini, Mchungaji Spear Mwaipopo, amesema Kanisa
litaendelea kuliombea Taifa na viongozi wake, lakini akawataka viongozi
wa nchi hii nao watimize wajibu wao kwa kutenda haki.
Alitoa kauli
hiyo jana wakati akizungumza na waumini wa Kanisa la Tanzania Assemblies
of God (TAG) lililopo Mwenge jijini Dar es Salaam katika ibada ya
kuadhimisha miaka 75 ya Kanisa hilo nchini.
Mchungaji Mwaipopo
ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo alisema; "Kama kanisa
tutaendelea kuliombea Taifa, lakini na Viongozi wa nchi hawana budi
kutimiza wajibu wao wa kulitendea haki Taifa letu kwa kudumisha
Muungano, amani na mshikamano na kutupatia Katiba bora inayotokana na
maoni ya wananchi."
"Sasa hivi kuna mabishano ya kiitikadi
yanayoendelea na sisi tusingependa kuwa na Katiba ya Chama bali ya
Watanzania wote... hakuna chama chenye watu zaidi ya milioni 45.
Tukiruhusu hali hii tutakuwa hatuwatendei haki Watanzania walio wengi,"
alisema.
Alisema kila jambo jema hushuka kutoka kwa Baba wa mianga
na kwamba kama Kanisa wamekuwa wakiliombea jambo hilo, hivyo anaamini
kwamba Mungu atalisimamia hadi mwisho.
Aliwataka waumini wa Kanisa
hilo kuendelea kuomba bila kuchoka. "Kwa hiyo wapendwa msiangalie
malumbano tu ndani ya TV, bali endeleeni kuomba ili jambo hili
aliloliazimia Bw. Liweze kutimia," alisema.
Alisema anafurahishwa na
ukweli kwamba Kanisa la TAG linaadhimisha miaka 75 wakati Taifa la
Tanzania limetimiza miaka 50 hapo jana tu (Aprili 26, 2014).
"Nawapongeza
Marais wetu wastaafu hayati Mwl. Nyerere na Abeid Amani Karume kwa
kudumisha Muungano wetu na kuruhusu kikatiba uhuru wa wananchi kuabudu.
Kudumu kwa Muungano kumetusaidia kuweza kuhubiri Injili hadi Zanzibar,"
alisema.
Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG-Taifa)
lilianzishwa mwaka 1939 na kanisa la kwanza hapa nchini lilijengwa
katika kijiji cha Igale, mkoani Mbeya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni