Powered By Blogger

Jumatatu, 18 Novemba 2013

Kwanini nguvu za kanisa la kwanza hazionekani katika kanisa la leo?

Kwanini nguvu za kanisa la kwanza
 hazionekani katika kanisa la leo?
Naianza mada mpya kwa swali gumu na linaloweza kuibua mijadala mingi huko tuendako; lakini ambayo itakuwa ni changamoto historia ya kanisa sanjari na madhehebu ya Kikristo yaliyopo ulimwenguni kwa sasa. Kwa wasomaji wangu wa miaka mingi, mtakumbuka huko nyuma, niliwahi kuandika makala yenye kuchambua tofauti zilizopo kati ya “madhehebu ya Kikristo” na “Ukristo halisi”. Ninalazimika kurudi katika uchambuzi wenye mwelekeo huo; lakini lengo kamili likiwa ni kudhihirisha kimaandiko na kihistoria kuhusu kitendawili cha miaka mingi kuhusu tofauti kubwa iliyopo kati ya nguvu za kanisa la kwanza na udhaifu wa kanisa la leo. Najua kuna utetezi ambao umekuwa ukitolewa na kurasimishwa kama ndio sababu kamili. Lakini matukio ambayo yamejitokeza katika karne za hivi karibuni yanaufanya utetezi uliokuwepo kupoteza ushawishi; na hivyo kutoa mwanya wa kufanya upya utafiti wa kimaandiko na kihistoria; ili kupata majibu sahihi ambayo hayatapingika hata kama yasiyopokubaliwa kwa haraka. Katika kujenga msingi thabiti wa mada hii, nitaanza kwa muhtasari kuchambua kwanza tofauti kati ya “Ukristo” na “Madhehebu ya Kikristo”:
Tafsiri ya misamiati ya “Ukristo”
na “Madhehebu ya Kikristo”
Kwa msomaji mpya unaweza kudhani ninataka kukuchanganya kwa kusema kuna tofauti ya Ukristo halisi na Madhehebu ya Kikristo. Pengine wewe unafikiri vyote ni kitu kile kile, chenye maana moja, ila majina tu ndiyo yanatofautiana. Tusisahu pia kwamba tofauti za maneno zinatosha kuleta maana tofauti ya maneno husika. Nivumilie tu nijieleze ili unielewe na kujua kule ninakoelekea.
Tafsiri ya awali nainukuu katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu, ili kupata maana ya maneno mawili ambayo, ni “Ukristo” na la pili “Madhehebu”. Maana za maneno haya zitatupa picha ya tofauti zilizopo kisha tunaendelea na uchambuzi kutoka vyanzo vingine vya lugha.
Kamusi ya Kiswahili Sanifu imelitafsiri neno “Ukristo” kuwa ni: “Dini inayoamini kuwa Mungu ni mmoja, inayofuata mafundisho ya Yesu Kristo.”
Hapa neno Ukristo limetafrisiwa kuwa ni dini. Hapa inaonesha kwamba Ukristo umejumuishwa na dini nyingine kama vile Uislamu na Ubudha.
Tunapokuja kwenye msamiati wa neno “Madhehebu” tunakuta Kamusi ya Kiswahili Sanifu imelitafsiri katika maana tatu zifuatazo: 1. Fikira na mwongozo wa kidini unaotokana na uelewaji wake wa misingi ya dini hiyo na unaoleta tofauti ndogondogo za mawazo lakini zisizovunja misingi ya dini hiyo. 2. Wafuasi wa mawazo ya kiongozi wa dini. 3. Mwenendo fulani wa kufanya au kuendesha mambo.
Tukichukua tafsiri ya kwanza na kuihusisha na msamiati wa madhehebu ya Kikristo inaweza kusomeka kama ifuatavyo: “Madhehebu ya Kikristo ni fikira au miongozo ya kidini inayotokana na uelewaji wake wa misingi ya dini ya Kikristo na inayoleta tofauti ndogondogo za mawazo lakini sizizovunja misingi ya dini hiyo ya Kikristo.”
Tukichukua tafsiri ya pili na kuihusisha na msamiati wa madhehebu ya Kikristo inaweza kusomeka kama ifuatavyo: “Wafuasi wa mawazo ya viongozi waasisi wa madhehebu katika dini ya Kikristo.”
Mpaka hapo, tukizichukua maana za maneno yaliyotajwa ya, “fikira”, “Mawazo” “Miongozo inayoleta tofauti ndogondogo za mawazo” tunaweza kufikia muafaka kwamba maana ya jumla ya Kiswahili kuhusu  madhehebu ya Kikristo inaweza kusomeka kama ifuatavyo: “Itikadi za kimakundi zilizoasisiwa na viongozi mbali mbali wa madhehebu ya Kikristo yanayotumia mwavuli wa dini ya Kikristo
Tukiishia katika maana iliyotokana na Kamusi ya Kiswahili Sanifu, tutakomea katika uelewa kwamba, madhehebu ya Kikristo na Ukristo ni kitu kimoja lakini chenye tofauti ndogondogo zinazotokana na mawazo ya viongozi wa makundi husika.
Je! Hii ndio maana yake halisi? Je! Tafsiri ya Kiswahili iliyopo imechukua maana sahihi ya maneno husika kutoka kwenye vyanzo sahihi vya lugha nyingine zilizotangulia kutumia maneno haya?
Kimsingi, tukitaka kujua maana sahihi ya neno, hususani lile lililoazimwa kutoka katika lugha nyingine, ni muhimu kurejea kwenye lugha asilia na kujifunza matumizi asilia ya neno hilo kabla halijahamishiwa katika lugha nyingine. Na hii ndiyo kazi nataka tuifanye hivi sasa katika uchambuzi wa maneno ya “Ukristo” na “Madhehebu ya Kikristo” jinsi yalivyotangulia kutumika kwenye lugha asilia kabla hayajahamishiwa katika Kiswahili chetu.
Chimbuko la msamiati ya “Ukristo”
Katika maandiko matakatifu ya Agano Jipya hakuna msamiati wa neno “Ukristo”. Kuna maneno mawili yafuatayo: 1. Kristo, na 2. Mkristo. Maana ya neno la kwanza la Kristo ni “Christos” likimaanisha “mpakwa mafuta”. Neno la pili la “Mkristo” kwa lugha asilia ni: “Christianos” likimaanisha “mfuasi wa Kristo”. Neno hili lilitajwa kwa mara ya kwanza mnamo karne ya pili ambapo watu wa mataifa waliamua kuwaita wenye kumwabudu Yesu kuwa ni “Wakristo
“hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia.” (Mdo.11:26)
Mara ya pili tunakutana na msamiati wa neno “Mkristo” wakati Paulo alipokuwa akijitetea mbele ya kiongozi katika dola ya kirumi jina lake Agripa. Huyu alisikiliza utetezi wa kiimani wa Paulo akajikuta anashawishiwa kufanyika mfuasi wa Kristo mpaka akamwonya Paulo kwa maneno yafuatayo:
“Agripa akamwambia Paulo, kwa maneno machache wadhani kunifanya Mkristo.” (Mdo.26:28)
Mara ya tatu tunakutana na msamiati wa neno “Mkristo” wakati Petro alipokuwa akiwausia na kuwatia moyo wafuasi wa Kristo ili kila Mkristo atetee imani yake hata kama yu katika mateso isivyo halali:
“Lakini ikiwa kwa sababu ni Mkristo asione haya, bali amtukuze Mungu katika jina hilo.” (1 Pet.4:16)
Kufuatia nukuu za maandiko kuhusu msamiati wa neno “Ukristo” tumebaini neno hili halijaandikwa kwenye nyaraka za Agano Jipya. Badala yake tumekutana na maneno ambayo yanafanana na huenda ndiyo yaliyosababisha kuzaliwa kwa msamiati wa neno “Ukristo”.
Hapa tunajifunza kwamba, msingi na chimbuko la “Wakristo” na “Mkristo” ni Yule mwenye jina hilo tangu mwanzo ambaye ni Yesu Kristo. Huko Antiokia, wanafunzi wa Yesu, badala ya kuendelea kuitwa kwa jina refu la wanafunzi wa Yesu Kristo” wakapewa jina fupi la ”Wakristo” lenye kuonesha moja kwa moja mahusiano yaliyopo ya kiimani kati yao na Kristo mwenyewe. Huko Baadaye neno “Mkristo” lilitumika kumtambulisha mwamini mmoja mmoja.
Katika historia ya mwanzo wa matumizi ya maneno haya “Wakristo” na “Mkristo” hatusomi habari za “mawazo” au “itikadi za kimakundi” katika imani ya Kikristo. Waliotajwa kutumia maneno haya hatusomi kwamba yalikuwa ni majina ya kimakundi au kiitikati zenye “tofauti ndogondogo” za mawazo ya waasisi wa kiimani. Ni maneno yaliyobadilika kuwa majina ya kundi lile lile moja, lenye imani moja, ubatizo mmoja, Bwana mmoja, ambalo lilikuwa likiongezeka idadi na kuenea katika miji na nchi mbali mbali za ulimwengu wa karne ya kwanza.
Kwa bahati mbaya, katika nyaraka za asili za Agano Jipya, hatuna msamiati wa neno, “madhehebu ya Kikristo” kwa maana ya tafsiri ile tuliyoipata kwenye Kiswahili chetu isemayo: “Itikadi za kimakundi zilizoasisiwa na viongozi mbali mbali wa madhehebu ya Kikristo yanayotumia mwavuli wa dini ya Kikristo
Kwa mantiki hii, kinachoweza kutusaidia kujua chimbuko la msamiati wa madhehebu ya Kikristo kwa maana ya “itikadi za kimakundi” katika imani ya Kikristo, si kingine bali ni historia ya kanisa, ambayo tunaendea kuipitia kwa ufupi kama ifuatavyo:
Chimbuko la “Madhehebu ya Kikristo”
Katika karne za kwanza za historia ya Ukristo, hakukuweko kabisa “madhehebu ya Kikristo” kama tuliyo nayo hivi leo. Japokuwa zilijitokeza changamoto za kuibuka kwa vijikundi vilivyokuwa vikijimega, vingi vilikuwa vidogo na wafuasi wake waliitwa “Wazushi” wala hawakuhesabiwa kuwa ni sehemu ya Ukristo. Tangu kipindi cha mwanzo wa Ukristo  kulikuwepo kanisa moja tu la “Katoliki” kwa maana ya “kanisa la ulimwengu mzima”. Kimsingi, mwamini yeyote ambaye hakuwa mshirika katika kanisa hilo hakutambuliwa kuwa ni Mkristo.
Historia ya “Madhehebu ya Kikristo” inaanza na kitu kinachoitwa “Mgawanyiko wa kanisa”. Mngawanyiko wa kwanza mkubwa ulijitokeza kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 1054 uliotokana na “Great Schism” kati ya Kanisa la Mashariki na Kanisa la Magharibi. Kuanzia hapo kukawepo makundi makubwa mawili ya kikristo ambayo baadaye yalikuja kujulikana kama Kanisa Katoliki la Magharibi na kanisa la Mashariki la Orthodox
Mgawanyiko mkubwa wa pili wa kanisa ulitokea katika karne ya 16 wakati wa Matengenezo Kiprotestanti ambayo mwasisi wake alikuwa Martin Luther. Katika kuonesha kutokuridhishwa kwake na mwenendo wa imani ya Kanisa mnamo mwaka 1517 alichapisha na kubandika mambo 95 (Thesis) ambayo hatimaye mnamo mwaka 1529 yalianzisha rasmi vuguvugu la Uprotestanti.
Hoja ya msingi iliyoleta mgawanyiko ni madai ya uhuru wa kuyatafsiri mambo ya imani na wokovu wa Mungu kama jambo linalomhusu mtu binafsi na Mungu, pasipo kupitia kwa mtu au taratibu za kitaasisi zenye kusimamiwa na binadamu.
Katika kuweka mkazo wa jinsi hii, wa uhuru wa kila mtu kujitafsiria maandiko na kusimama mbele za Mungu kwa imani yake, kukaligawa kanisa na kuwa na makundi mawili ambayo ni “Uporotestanti” na “Ukatoliki”. Kundi la Ukatoliki likaendelea na msimamo wake kwamba wa tafsiri ya maandiko na mafundisho kuwa chini ya udhibiti wa utawala wa kanisa ili kuepusha kuwachanganya wafuasi kwa sababu ya kila mtu kujitafsiria mambo yake binafsi.
Kundi lililomeguka kutoka kwenye “Ukatoliki” lenyewe likaendeleza vuguvugu lake jipya la kupinga kwamba utaratibu wa kudhibiti tafsiri ya maandiko tayari kulikwisha kusababisha uharibifu wa imani ya kweli ya Ukristo. Likaendelea kusisitiza kwamba waamini wapewe uhuru wa kujisomea maandiko wenyewe na kuyatekeleza kwa jinsi wanavyoongozwa na dhamiri zao wenyewe.
Vuguvugu la matengenezo lilipoanza huko Ujerumani, ndipo makundi mengine katika sehemu za Ulaya nayo yakaanza kumeguka kutoka katika Kanisa Katoliki. Wakajitokeza wana-matengenezo kama Ulrich Zwingli na John Calvin na John Knox ambao waliasisi makundi ya kimethodist, Presbyterian, wabaptisti na kadhalika.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni